WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
Tanzania kama nchi inapaswa kuwa na mpango wa kuendeleza mipango miji
(master plan) wa nchi nzima unaozingatia ukuaji wa miji yetu.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumatatu, Novemba 10, 2014) wakati akifungua warsha ya siku tatu ya
kuwajengea uwezo Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za
Wilaya na Manispaa za Miji kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
“Sasa hivi hapa nchini tuna
tatizo la ukuaji mkubwa wa miji yetu na Dar es Salaam ni mmojawapo.
Hakuna miundombinu ya majitaka, nyumba zimesongamana, hakuna barabara za
uhakika… ukuaji wa miji ni lazima uangaliwe kwa naman ya tofauti na
upewe uzito unaostahili,” alisema.
Lazima tuje na master plan ya
miji yote mikubwa kama Arusha, Mwanza na Dar es Salaam hata kama
itabidi kutafuta wafadhili ili tuweze kuifanya kazi hiyo. Lazima huo
mpango kabambe uwepo kama kweli tunataka kumaliza tatizo hili,”
aliongeza.
“Hivi hata ukitaka kupeleka timu
ya waokoaji unawapelekaje? Je ukiwapeleka wapite wapi?, watue wapi?
Lazima tutafute wafadhili wa kufinance mpango huu,” alisisitiza.
Akitoa mfano Waziri Mkuu alisema
kukosekana kwa mipango miji kunaleta matatizo ya wnanchi kupelekewa
mahali hata kama hapajaandaliwa. “Kulitokea mafuriko hapa Dar es Salaam,
watu wakapelekwa Mabwepande. Je kulikuwa na mpango wowote wa
miundombinu ya kuwaweka huko? Je, yakitokea mafuriko mengine, watu
watapalekwa wapi?” alihoji.
Alisema kutokuwepo kwa mpango huo kumefanya asilimia 70 ya makazi kujengwa katika maeneo yasiyo rasmi.
Waziri Mkuu pia aliwataka
viongozi hao waangalie ni kwa jinsi gani wanaweza kupunguza athari
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo wanakotoka.
“Kwangu mimi natamani kuona madhara yanayotokana na tabianchi
yakipungua. Jaribuni kujiuliza mtaweka mikakati gani ili kupunguza
athari za mafuriko,” alisisitiza.
Aliwataka pia waangalie athari za
uchafuzi wa mazingira kwa sababu ni changamoto kubwa katika miji mingi
hapa nchini. “Pale Kinyerezi wana dampo na wanaona suluhisho ni kuchoma
moto lakini hawaangalii madhara ya ule moshi unaotokana na uchomaji
taka,” alionya.
Mapema, akielezea kuhusu mkutano
huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Eng. Mussa Natty alisema
mkutano huo umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano (Durban
Adaption Charter) yaliyofanyika jijini Durban, Afrika Kusini, Desemba,
2011 ikiwa ni sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la mabadiliko ya
tabianchi.
“Wakati tulipoenda Durban,
tulienda na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Manispaa ya Temeke. Sasa hivi ziko Halmashauri 102 ambazo zimeshatia
saini makubaliano haya,” alisema.
Lengo la mkutano huo ni kutafuta
njia za kutafuta ufumbuzi wa mabadiliko ya tabia kwa kutumia mbinu
zinaoendana na mazingira ya hapa nchini (local solutions).
0 comments:
Post a Comment