Tanzania na China, zimetiliana
saini mkataba wa maelewano (MoU) ambapo taasisi za China zitawekeza mabilioni
ya dola za Marekani katika uchumi wa Tanzania.
Shughuli
ya utiaji saini imekuwa sehemu ya mkutano wa tatu wa uwekezaji kati ya Tanzania
na China uliofanyika ukumbi wa mikutano wa nyumba ya wageni ya serikali ya
Diaoyutai mjini Beijing, China.
Aidha,
utiaji saini huo ambao utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na
mitaji na uwekezaji kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya kiserikali ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Kikwete China kwa mwaliko
wa Rais Xi Jinping.
Miongoni
mwa makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na ushirikiano wa kimkakati kati ya
Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na kampuni ya China Railway Jianchang
Engineering (CRJE) ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika
uchumi wa Tanzania.
Kiasi
cha dola bilioni moja zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa Salama Creek
Satellite, eneo la Uvumba, wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na kiasi cha dola
milioni 500 zitawekezwa katika ujenzi wa Financial Square, eneo la Upanga.
Aidha,
NHC itapata kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kutoka kampuni ya Poly
Technologies kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es
Salaam.
Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limetiliana saini makubaliano na kampuni ya
Hengyang Transformer ambapo kampuni hiyo itapata mamilioni ya dola za Marekani
kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme vijijini.
Aidha,
TANESCO limetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi
IV.
Halmashauri
ya manispaaa ya Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini makubaliano na kampuni
ya Jiangyin Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kikwete
Friendship Highway katika wilaya ya Temeke.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sofia
Mjema, walishuhudia utiaji saini makubaliano hayo.
Vile vile, mkoa wa Pwani, umetiliana saini makubaliano na
kampuni ya Jiansu Shenli Plastics Group Limited ya China kwa ajili ya
kugharamia na kuendeleza mradi wa viwanda na uchumi katika eneo la Mlandizi.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mwantumu Bakari Mahiza, alitia
saini kwa niaba ya mkoa wake.
Wakati huo huo Rais Kikwete, alisema maendeleo ya haraka
ya China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za Afrika kuwa nazo zinaweza
kuendelea katika kipindi kifupi kama zitaongozwa na sera sahihi za mageuzi ya
kiuchumi.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati alipokutana kwa
mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la China, Zhang Dejiang, ikiwa
ni moja ya shughuli za Rais katika ziara yake rasmi ya China.
Katika mazungumzo hayo kwenye jengo la Bunge la Great
Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete alimwambia Dejiang: “China
inatuhamasisha kwamba na sisi tunaweza kupata mabadiliko na maendeleo ya haraka
ya wananchi wetu ili mradi tu tuweze kuwa na sera sahihi ambazo zinalenga
katika kuleta mageuzi ya msingi na ya kweli kweli ya kiuchumi”.
Alisema kwake yeye ambaye amekuwa anatembelea China kila
baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya China yanatia hamasa kweli kuwa
nchi za Afrika pia zinaweza kuleta mageuzi makubwa ya maisha ya watu wake.
“Nilikuja hapa kwa mara ya kwanza mwaka 1980, na tokea
wakati huo nimetembelea nchi hii kila baada ya miaka minne kwa wastani na kila
nikija nashuhudia mabadiliko makubwa yasiyopimika na wala kufikirika. China
ilikuwa nchi masikini sana wakati nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini
katika miaka 30 tu imebadilika kutoka nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea
na yenye uchumi unaoshikilia nafasi ya pili kwa ukubwa duniani,” alisema.
“Tunawapongeza kwa juhudi ambazo zimewafikisheni hapa.
Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo siku moja na sisi katika Afrika tutafikia hatua
hii ya maendeleo,” alisema.
Naye Dejiang alimkubusha Rais Kikwete mazungumzo kati yao
wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita Ikulu, mjini Dar es
Salaam.
Wakati huo, Dejiang alikuwa Katibu wa Chama Tawala cha
Kikomunisti cha China katika jimbo la Guangzhou, jimbo ambalo linaongoza katika
China kwa kufanya biashara na Tanzania.
Kati ya biashara zote ambazo Tanzania na China zinafanya,
asilimia 60 inatokea jimbo la Guangzhou.
Alipongeza uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China
katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kibalozi Aprili 26,
mwaka 1964.
Pia alisema ujenzi wa Reli ya TAZARA unaendelea
kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania na Zambia na kuongeza kwa
Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia maanani utajiri na raslimali
zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia, utulivu na amani na idadi kubwa ya
watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi tajiri katika miaka isiyokuwa mingi ijayo.
0 comments:
Post a Comment