Watoto wa Mitaa ya Mwanjelwa na Soweto
timu ya Mbeya City kutoka Mkoani Mbeya, tayari imekamilisha usajili wa
Mshambuliaji kutoka Timu ya Kagera Sugar Themi Felix na Kiungo Peter
Mwalianzi kutoka timu ya JKT Mgambo.
Safu ya Ushambuliaji ya Timu hiyo
iliyofanikiwa kushika Nafasi ya Tatu kwenye Ligi Kuu Vodacom, VPL, Msimu
huu, itakuwa sasa na Paul Nonga, Mwagane Yeya, Saad Kipanga na Themi
Felix kuanzia msimu ujao na huku Peter Mwalianzi akiongeza nguvu kwenye
safu ya Kiungo inayoongozwa na Steven Mazanda.
Nao Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC,
tayari walishakamilisha usajili wa Frank Domayo na Didier Kavumbagu
kutoka Yanga na kumuongeza Beki Abdallah Heri kutoka Klabu ya Zimamoto
ya kule Zanzibar.
Kwa sasa safu ya Kiungo ya Mabingwa
hao itaundwa na Himid Mao, Kipre Balou, Salumu Abubakary na Domayo Frank
huku Brian Umony, Gaudence Mwaikimba, John Bocco, Kipre TcheTche na
Kavumbagu wakikamilisha Safu ya Ushambuliaji.
Timu ya Ruvu Shooting iliyomaliza
Msimu kwenye Nafasi ya Tano baada ya kupata Alama 38, tayari
imekamilisha usajili wa Zuberi Dabi kutoka Klabu ya Kagera Sugar. Timu
hiyo pia imefanikiwa kumsajili Chagu Chagula mshambuliaji Raia wa
Tanzania ambaye amecheza sana Nchini Burundi.
Baada ya kuandaa mkakati na kuachana na
Wachezaji wanaotemwa na Timu za Simba na Yanga, Klabu ya Coastal Union
ya Tanga tayari imekamilisha usajili wa Bright Obina ambaye aliwahi
kuzichezea African Lyon na Ashanti United zote za Dar es Salaam.
Timu hiyo pia imefanikiwa kumnasa
Hussein Swed ambaye Msimu uliopita alikuwa na Timu iliyoshuka Daraja ya
Ashanti United na sasa wote wametua kwa Wagosi wa Kaya.
Kwa mujibu wa TFF, Usajili wa Wachezaji
kwa hatua ya kwanza Msimu mpya wa 2014/2015 unaanza Juni 15 hadi Agosti 3
Mwaka huu wakati Kipindi cha kutangaza Wachezaji walioachwa au
kusitishiwa Mikataba ni kuanzia Juni 15 hadi 30.
Kipindi cha kwanza cha Uhamisho wa Wachezaji ni kuanzia Juni 15 hadi Julai 30.
Kupitia Majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Agosti 4 na 11 na kuthibitisha Usajili hatua ya awali ni Agosti 12 hadi 14.
Usajili hatua ya pili utakuwa kati ya
Agosti 14 na 29 wakati kupitia na kutangaza Majina ya pingamizi hatua ya
pili ya usajili ni kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4. Uthibitisho wa
Usajili hatua ya pili ni Septemba 5 na 6.
Ligi Kuu ya Vodacom, VPL, inatarajiwa kuanza Agosti 24 na Ratiba inatarajiwa kutoka Mwezi mmoja kabla hapo Julai 24.
0 comments:
Post a Comment