Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter
Pinda kuomboleza kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa,
Ndugu Moshi Chang’a(pichani).
“Ni
kifo cha kusikitisha kwa sababu kimepunguza safu ya uongozi wetu na
kimelinyang’anya taifa letu mhamasishaji hodari na mtetezi wa kuaminika
wa maendeleo ya wananchi,” Rais Kikwete amesema katika salamu hizo.
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi: “Nilimjua
Ndugu Chang’a kwa miaka mingi tokea mwaka 1979 alipojiunga na utumishi
wa Chama cha Mapinduzi ambacho pia alikitumia kwa uaminifu mkubwa hadi
alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mwaka 2003. Alikuwa kiongozi wa kweli
kweli wa maendeleo na kifo chake kimetuachia pengo la uongozi.”
“Nakutumia
salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako,
naitumia familia wa Ndugu Chang’a pole za dhati ya moyo wangu kwa
kuondokewa na mzazi na mhimili wa familia. Nakuomba uwajulishe kuwa
naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na
uvumilivu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao
katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya
marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.
Ndugu Moshi
Chang’a ambaye aliaga dunia jioni ya, Jumapili, Aprili 20, 2014 katika
Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar Es Salaam amekuwa mkuu wa wilaya
katika Mikoa ya Mbeya, Tabora na Rukwa.
0 comments:
Post a Comment