Home » » MKUU WA MKOA WA MARA AFARIKI DUNIA

MKUU WA MKOA WA MARA AFARIKI DUNIA


MKUU wa Mkoa wa Mara, John Tupa amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla akiwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime wakati akiendesha kikao.
Tupa alikwenda wilayani humo kwa ajili ya kufunga mafunzo ya mgambo katika Kijiji cha Nyamwaga.
“Alianguka chini, akazimia baadaye tukamkimbiza hospitalini ili kuokoa maisha yake. Lakini wakati madaktari wakiendelea kumhudumia kwa kumpa dawa nyingine anazopewa mtu anayepata presha, lakini kwa muda kama wa saa moja akiwa pale hospitalini, tukiwa tunapanga mambo mbalimbali ya kumpeleka labda Bugando ama Musoma, mkuu wa mkoa akatutoka,” alisema Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Yacobo Shayo.
Mkuu wa Wilaya Tarime, John Henjewele alisema Tupa alianguka kutoka kwenye kiti ofisini kwake wakati akiendesha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na mkoa huo kabla ya kwenda na ujumbe wake kufunga mafunzo hayo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Dk Marko Mega, alisema alifariki dunia jana asubuhi muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Tarime, Maiko Negga alithibitisha kifo hicho kimetokana na shinikizo la damu.
Mshauri wa Mgambo wa Wilaya ya Tarime, Mgaya Ezekiel alisema mkuu huyo wa mkoa, ndiye aliyekuwa anasubiriwa kufunga mafunzo hayo yanayoshirikisha mgambo 313. Ilikuwa ayafunge saa 2:00 asubuhi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamwaga, Kirigiti Sasi, alisema pamoja na kufunga mafunzo ya mgambo, mkuu wa mkoa alitarajiwa kufungua ofisi ya kijiji hicho.
Sasi alisema kazi hiyo itapangiwa siku nyingine na kuelezea kifo hicho, ni pigo kubwa kwao. Rais aomboleza Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kutokana na kifo hicho.
Rais Kikwete amemwomba Waziri Ghasia amfikishie salamu za pole kwa familia ya marehemu Tupa kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Mazishi Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, taratibu na maandalizi ya mazishi zinafanywa kwa ushirikiano wa familia, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi. Tupa alizaliwa Januari Mosi, 1950.
Amewahi kuwa Mkuu wa wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mwaka 2011. Ameacha mjane na watoto watano.
Habari hii imeandikwa na Hamed Makongo na Samson Chacha, Tarime.







0 comments:

Post a Comment

TANGAZA NASI | 0783 561 514

 
Idrisa Bandali Available On : Facebook | Instagram | Twitter
Copyright © 2013. BANDALI 44 -Haki Zote Zimehifadhiwa
Blog Hii Imetengenezwa Na Ernest James Siwigo Inamilikiwa Na Idrisa Bandali
2brothers Inc 0719766915 | 0764214303